Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule
Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga
linamshikilia diwani wa kata ya Bunambiu wilayani Kishapu Richard
Sangisangi(48) kupitia Chama Cha Mapinduzi kwa kumshambulia kwa kumpiga
ngumi usoni na kifuani muuguzi wa kituo cha afya Bunambiu Hilda Simon
(35).
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari
leo,Machi 9,2018 Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule
alisema Sangisangi alimpiga muuguzi huyo katika kituo cha afya Bunambiu
na kumsababishia maumivu makali.
Alisema chanzo cha tukio hilo
lililotokea Machi 8,2018 majira ya saa tatu na nusu asubuhi ni diwani
huyo kutokuwa na na imani na muuguzi huyo wakati akiwahudumia wagonjwa
hivyo kuamua kumshambulia kwa kumpiga ngumi.
“Mtuhumiwa tumemkamata na
tutamfikisha mahakamani mara tu baada ya taratibu za kiupelelezi
kukamilika,natoa wito kwa wananchi na viongozi kuacha kujichukulia
sheria mkononi”,alisema kamanda Haule.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio
hilo,waliiambia Malunde1 blog kuwa diwani huyo alimtuhumu muuguzi huyo
kuwa hahudumii wagonjwa vizuri na kumtaka aondoke kituoni na alipogoma
ndipo diwani alipoamua kumshambulia mbele ya wagonjwa.
Walisema diwani huyo alipigiwa simu na
wananchi wakimwelezea kuwa mgonjwa wao aliyelazwa katika kituo hicho cha
afya hapatiwi huduma vizuri na ndipo diwani huyo alipoomba kuongea kwa
simu na muuguzi wa zamu,muuguzi akamsihi diwani afike kituoni na
alipofika akaanza kumshambulia muuguzi huyo.
“Huyu diwani alipigiwa simu na ndugu wa mgonjwa,kwamba mgonjwa wao hapatiwi huduma vizuri hali inayosababisha aendelee kulazwa”,walieleza.
Hata hivyo habari zaidi zinasema,wakati
Hilda Simon akiendelea kuhudumia wagonjwa,ghafla muuguzi mwingine ambaye
hakuwa zamu aliingia katika wodi ya wagonjwa na kuwaambia ndugu wa
mgonjwa huyo kuwa ndugu yao ana upungufu wa damu hivyo anatakiwa kupewa
rufaa kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
“Kutokana na hali hiyo ndipo ndugu wa
mgonjwa wakaamua kumpigia simu diwani na kutaka kuongea kwa simu na
nesi wa zamu,nesi akaomba diwani afike ofisini,alipofika ndipo akaanza
kuonesha ubabe kwa kumshambulia muuguzi ambaye alikuwa zamu na alikuwa
anasimamia kituo cha afya kutokana na mganga mkuu wa kituo kutokuwepo
kazini”,walisema mashuhuda wa tukio hilo.
Tukio hilo limetokea wakati wanawake wakisherehekea siku ya wanawake duniani.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog
No comments:
Post a Comment